Mwenyekiti wa kitaifa wa mpango ya Nyumba Kumi Joseph Kaguthi, amewataka Wakenya kuondoa fikra kuwa Waislamu ni magaidi.
Akizungumza na wanahabari jijini Mombasa, Kaguthi alisema kuwa kuna haja ya uwiano miongoni mwa wafuasi wa dini mbalimbali, ili kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa ukanda wa pPwani na Kenya kwa jumla.
“Tuungane pamoja kama ndugu na kukabiliana na ugaidi kote nchini ili kuimarisha usalama,” alisema Kaguthi.
Aidha, Kaguthi alisema kuwa kuna haja ya ushirikiano kati ya wananchi na idara za usalama, ili kukabilina na tatizo la ugaidi na itikadi kali.
“Tukishirikana na polisi, basi usalama utaimarika na hakutakuwa na visa vya ugaidi na wizi,” aliesema Kaguthi.
Wakati huo huo, amesema kuwa kuna haja ya vyombo vya habari kuhakikisha kuwa hawaripoti maswala ya ugaidi kwa haraka, na kusubiri ripoti kutoka idara ya usalama, kwa vile magaidi hufurahia wanapotekeleza mikasa hiyo.
Mkutano huo ulijumuisha viongozi mbalimbali kutoka kaunti za Kilifi, Kwale na Mombasa ambao wanalenga kuelimisha jamii mashinani kuhusu umuhimu wa kudumisha usalama na amani.