Kikundi cha amani na maridhiano na viongozi kutoka dini ya kiislamu katika kaunti ya Uasin Gishu walifanya mkutano siku ya Jumanne ili kuzungumzia maswala ya ugaidi katika kaunti hiyo.
Mkutano huo uliojumwisha viongozi wa kiislamu kutoka kaunti ya Nandi na UasinGishu, ulifanywa ili kuwaleta pamoja wananchi kutoka dini na jamii mbalimbali nchini Kenya pasipo kuzingatia msingi wa kikabila au dini.
Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya kaunti hiyo, David Busienei, Mwenyekiti wa kikundi cha amani na maridhiano, alisema kwamba nchi inakabiliwa na changamoto ya ugaidi, na kwamba ugaidi unafaa uchukuliwe kama kosa la jinai wala sio tendo la dini ya kiislamu.
“Serikali inafaa ichukue hatua ya kuwachunguza magaidi wote nchini na kuwachukulia hatua ya kisheria,” alisema.
Mohammed Jama, mwenyekiti wa jamii ya kisomali katika kaunti ya Uasin Gishu alisema kwamba kundi la kigaidi la Alshabaab sio shirika la kiislamu, bali ni shirika la kigaidi wala hawashiriani kwa vyovyote vile na wao.
“Magaidi hao wana nia ya kuwagawanya wakenya kwa misingi ya kidini na kikabila, mtu yeyote hapaswi kumwogopa mwislamu kwani waislamu si alshabaab,” alisema Jama.
Aidha, Jamah ameomba viongozi kuwa makini sana wanapozungumza kwenye mikutano, ili wasiwachochee wakenya kwa njia itakayowafanya kuwachukulia waisilamu kwa njia isiyo sahihi.
“Serikali ifanye kila juhudi ili kurejesha amani nchini, na pia nawasihi waweze kushirikiana na viongozi wa dini ya kiislamu ili kuwashika magadi wanaovuruga amani nchini,”alisema Jama.
Kikundi cha amani na maridhiano kinapanga kufanya mikutano mingine kote nchini ili kueneza ujumbe wa amani.