Zaidi ya wakaazi 4,000 katika eneo la Ganze wamenufaika na msaada wa chakula uliodhaminiwa na shirika la kuzalisha umeme nchini KenGen.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea katika zoezi la kugawa chakula hicho kilichowagharimu takribani shillingi milioni 1.5, kaimu mkurugenzi wa kampuni ya KenGen tawi la Mombasa, Bw Simon Kirui aliwataka wakaazi kushiriki njia mbadala ya kutafuta hela za kujikimu, badala ya kukata miti na kuchoma makaa.

"Zamani kulikuwepo na pori na hakukuwa na shida ya mvua lakini miaka 10 baadae, biashara ya makaa imekithiri, miti imekatwa kwa kiwango kikubwa sana na matokeo yake ni ukame unaowaumiza wakaazi," alisema Kirui.

Lokesheni tatu ndogo ikiwemo Dangarani, Nagoni na Goshi ndizo zilizonufaika na msaada huo.

Wakaazi walipokea unga wa mahindi kilo 48 kwa kila familia, mafuta ya kupikia, nafaka ikiwemo mchele na maharagwe.

Bw Kirui ameomba mashirika mengine pamoja na serikali kusaidia jamii zilizoathrika.

Hatahivyo, amesema kuwa ni muhimu kwa serikali kutafuta suluhu ya kudumu, na kuwataka wakaazi kubadili mbinu za kilimo.

“Ningependa kuwaomba wakaazi wabadili mbinu za kilimo kwa sababu wamekuwa wakipanda mahindi ambayo hayafanyi vizuri kulingana na mabadiliko ya mazingira na anga," alisema Kirui.