Wakaazi wa Bamburi, eneo bunge la Kisauni, wamelalamikia ukosefu wa maji katika eneo hilo.
Wakizungumza siku ya Alhamisi na mwandishi huyu, wakaazi hao walilalamikia ukosefu wa bidhaa hiyo muhimu na kuinyoshea kidole cha lawama kampuni ya usambaji maji ya Mombasa, kwa kutosikia kilio chao.
Wakiongozwa na Ali Mwakarimu, wakaazi hao waliwalaumu wanasiasa kwa kusema kuwa wameilitumia swala la ukosefu wa maji katika eneo hilo kama kigezo cha wao kutafuta kura, lakini pindi waingiapo madarakani, wao hulisahau tatizo hilo.
Aidha, wakaazi hao wameitaka kampuni ya usambazaji maji ya Mombasa kuwajibika na kuhakikisha kuwa wanapata maji.
“Tumehangaika kwa muda mrefu sana bila maji. Kila tunapolalamika, Kampuni ya usambazaji maji ya Mombasa huturejeshea huduma hiyo kwa muda, na baada ya siku chache, maji hupotea tena hata kwa muda wa mwezi mmoja,” alisema Mwakirimu.
Kampinu hiyo ilijitetea kwa kusema kuwa kiasi cha maji kinachohitajika Mombasa ni kikubwa ikilinganisha na maji yanayopatikana katika eneo hilo.
Hatahivyo, kampuni hiyo iliahidi kuwapa wakaazi huduma hiyo hivi karibuni kwa sababu ni jukumu na wajibu wao kama kapuni kufanya hivyo.