Zaidi ya wakaazi 300 wa eneo la Elementaita, kwenye eneo bunge la Gilgil, walifanya maandamano ya amani siku ya Jumatano kulalamikia hali mbaya ya barabara ya Elementaita.
Wakaazi hao waliandamana kwa zaidi ya kilomita 15 kutoka kituo cha kibiashara cha Jogoo hadi kwenye kituo cha kibiashara cha Elementaita, huku wakiwashtumu viongozi wao kwa kuwasahau.
Walikariri kuwa wamelazimika kuvumilia matukio ya magari yao kuharibikia barabarani pamoja na kuchelewa wanaposafiri kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Wakaazi hao walidai kwamba licha ya kuwarai viongozi waliowachaguwa kuwatengezea barabara hiyo, ni machache tu ambayo yamefanywa kukarabati barabara hiyo inayounganisha mji wa Gilgil na eneo la Maunarok mjini Njoro.
Baadhi ya madereva wa matatu waliohojiwa na wanahabari walisema wamelazimika kutengeza magari yao mara kwa mara huku wakiitaka serikali kuleta matinga aina ya ‘grader’ kuainisha barabara hiyo kabla ya kupata suluhu la kudumu.
Wakaazi hao walisema kwamba iwapo barabara hiyo itasalia katika hali hiyo katika muda wa wiki mbili zijazo, hawatakuwa na lingine ila kuanza harakati za uhamasishaji kuhakikisha kwamba walio uongozini kwa sasa hawachaguliwi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.
Barabara hiyo iliyoko chini ya mamlaka ya ujenzi wa barabara za mashambani ya Kenya Rural Roads Authority (Kerra) hutumika na malori kusafirisha vyakula vya shambani kutoka Maunarok Njoro, pamoja na mchanga unaotumika katika ujenzi kutoka eneo la Kiptangwanyi kwenye Kaunti ya Nakuru.