Wakaazi wa mtaa wa Freehold viungani mwa mji wa Nakuru, wamelalamikia barabara mbovu katika eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi hao walisema kuwa barabara ya Mashindano imejaa mashimo, hali inayosababisha maji kujaa barabarani wakati wa mvua.

Wakiwakilishwa na mwenyekiti wa Nakuru stakeholders Forum Wycliff Oguda, wakaazi hao waliitaka serikali ya Kaunti ya Nakuru kuelezea ni mwanakandarasi yupi aliyepewa kazi ya kutengeneza barabara hiyo, na kiasi cha fedha kilichotumika kukarabati barabara hiyo.

“Tunasikitika sana na kuhuzunishwa na serikali ya Kaunti ya Nakuru kwa kukosa kutushughulikia,” alisema Oguda.

Aidha, wakaazi hao waliitaka kampuni ya Kenya Power kuondoa mlingoti na nyaya za umeme zilizoanguka katika barabara hiyo kufuatia mvua kubwa iliyoshuhudiwa katika eneo hilo.

Wakaazi hao aidha walliikosoa kampuni hiyo kwa kuzuru eneo hilo na kukosa kuuondoa mlingoti huo barabarani.

Wakaazi hao walisema kuwa serikali ya Kaunti ya Nakuru inapaswa kuwajibika kwa kuwa ni jukumu lake kukarabati barabara zinapoharaibika.