Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuweka gari la zimamoto katika eneo bunge la Jomvu.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwa njia moja ya kuwaepusha wakaazi wa eneo hilo na uharibifu na hasara wanazokadiria wakati wa mikasa ya moto.

Wakizungumza siku ya Jumatatu, wakaazi hao wakiongozwa na afisa anayesimamia majanga katika eneo la Jomvu Bakar Nyundo, walisema kuwa kuna haja ya kuweko na gari la zimamoto katika eneo hilo ili iwe rahisi kukabiliana na mikasa ya moto kwa haraka.

Haya yanajiri baada ya moto kuteketekeza baa moja katika mtaa huo usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu, na kusababisha hasara ya mamilioni ya pesa.

Aidha, afisa huyo alisema kuwa kizuizi kilichoko kwenye barabara ya kuingia eneo la makaazi la Miritini kinachangia pakubwa kuchelewa kwa magari ya zimamoto kwa kuwa mengi huwa hayawezi kupita.

Vile vile, wakazi wa eeno hilo wamelitaka shirika la kusambaza umeme la KLPC kuhakikisha nyanya za umeme zimerekebishwa kwa muda ufaao ili kuepuka hasara zinazokadiriwa na wafanyibiashara.