Siasa zilishamiri hafla ya mchango wa fedha huko Kapkures Nakuru Alhamisi huku wakaazi wakidai wamepuuzwa na serikali ya Jubilee.
Wakiongozwa na Wesley Korir, wakaazi hao walisema kwamba serikali imewatelekeza.
"Sisi tuko serikalini kwa kuvumilia tu lakini tunafikiria kuhama iwapo serikali haitatukumbuka hapa Kapkures,"alisema Korir.
Walitoa wito kwa naibu gavana wa Nakuru Joseph Ruto kuangazia maslahi yao.
Isitoshe waliongeza kuwa atakapozuru tena Nakuru Rais Uhuru Kenyatta, wataamua kumweleza ukweli kwani wamechoka.
"Tumechoka na naibu gavana Ruto anafaa kujua sisi tumechoka na hatutakaa chini wakati mambo yanakwenda mrama,"alisema Korir.
David Karuri anayenuia kuwania kiti cha ubunge eneo la Nakuru Magharibi aliwapa changamoto viongozi wa Nakuru kushirikiana katika kufanikisha miradi ya maendeleo. "Kiongozi yeyote anayesimama wadhifa wowote anafaa kuwa na maono ya kuleta maendeleo Kwa jamii,"alisema Karuri.