Kulishuhudiwa kisanga katika kijiji cha Kinamba mjini Naivasha mapema Jumanne baada ya wakazi waliokuwa na gadhabu kusimamisha ujenzi wa zahanati iliyofadhiliwa na hazina ya ustawishaji maeneo bunge CDF.
Wakazi hao ambao pia walifanya maandamano, wamekashifu hatua ya mbunge wa eneo hilo John Kihagi na kamati yake ya CDF ya kutofuata sheria na kuanza kujenga zahanati ya umma kwenye ardhi ya kibinafsi.
Kwa wakati mmoja wakazi hao walitishia kuvua nguo zao ili kumlaani mbunge huyo huku wakisema kuwa walinunua ardhi hiyo mnamo mwaka wa 1981 na wamekuwa wakitumia uwanja huo kwa maswala ya zao la pareto.
Mmoja wao Grace Njoki alisema kuwa Kihagi alikuwa akitaka kunyakua ardhi hiyo kwani hawajahusishwa kwa vyovyote katika mipango inayofanywa.
Naye George Ngugi alisema kuwa: "Mbunge Kihagi alifanya mkutano nasi mwezi jana na hatukusikizana jinsi ya ununuzi na tumeshangaa ni kwa nini alianza kujenga zahanati hii kwenye ardhi yetu."
Juhudi za mwandishi huyu kujaribu kuwasiliana na mbunge huyo au hata afisi za CDF hazikufua dafu kwani simu zake hazikujibiwa.