Kufuatia kuchipuka kwa visa vya kihalifu mara kwa mara mjini Mombasa, maafisa wa polisi wameweka mikutano ya hamasa kuwashauri wakaazi kushirikiana nao kuimarisha usalama.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Kisauni Julius Kavita amesema kuwa jamii ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa usalama wa eneo lao unaimarishwa.

Aliongeza kwa kusema kuwa iwapo wazazi watawalinda vyema vijana wao na kuwashauri jinsi ya kujiepusha na makundi ya kihalifu, basi visa vya kihalifu vitapungua.

Akizungumza na wanahabari katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Kavita alisema lazima wakaazi kuzidisha ushirikiano wao na maafisa wa polisi ili kuyakabili makundi ya kihalifu kikamilifu na kuweka amani katika eneo hilo.

Aliwataka wakaazi kuwaripoti vijana wanaojihusisha na makundi ya Wakali Kwanza na Wakali Wao kwa maafisa wa polisi kwa kusema kuwa vijana hao wamekuwa tishio kwa wakaazi.

“Tunawashauri wakaazi na wazazi wa vijana waliojiunga na makundi ya kihalifu kuhakikisha kuwa wanawaripoti vijana hao kwa maafisa wa usalama mara moja la sivyo, polisi watayakabili makundi hayo,” alisema Kavita.

Afisa huyo aidha amewataka wazazi kushirikiana vyema na kuwalinda watoto wao sambamba na kuwapa elimu bora ili kuwasaidia katika siku za usoni.