Mwenyekiti wa kamati ya afya katika bunge la kaunti, ambaye pia ni Mwakilishi wadi Kisii ya Kati Wilfred Monyenye amewahimiza wakaazi kushirikiana pamoja kupambana na ugonjwa wa Ukimwi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa zaidi ya wakaazi 10,000 katika kaunti hiyo hujihusisha katika masuala ya ukahaba huku mji wa Kisii ukiandikisha idadi kubwa ya watu 6,000 ambao wamebobea katika ufuska.

Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Itibo kaunti ya Kisii, Monyenye alisema ili maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi yapungue sharti wakaazi washirikiane pamoja.

Monyenye alisema watu 9 na watoto 15 hufariki kila wiki kupitia ugonjwa huo.

“Naomba wakaazi wote wa Kisii tushirikiane tupunguze maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi," alisema Monyenye.

"Na wale ambao hufanya ukahaba katika sehemu mbalimbali za kaunti hii naomba muache maana jamii yetu itapungua,” aliongeza Monyenye.

Wakati huo huo , naibu gavana wa kaunti hiyo Joash Maangi aliomba wakaazi kujaribu kila wawezalo kuhakikisha wanazuia magonjwa kuliko tiba kwani wengi hutumia pesa nyingi katika matibabu.