Mbunge wa Nyaribari Masaba, Kaunti ya Kisii Elijah Moindi amewaomba wakaazi wa kaunti hiyo kuchukua hatua kwa Wabunge wanaoshukiwa kutumia vibaya pesa za hazina ya CDF.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea siku ya Jumanne katika ukumbi wa Cultural Hall mjini Kisii wakati wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu hazina ya CDF kusalia kuwa katika Serikali ya Kitaifa au iwe chini ya Serikali za kaunti, Mbunge Moindi aliomba wakaazi hao kuwashtaki  Wabunge ambao wanatumia pesa za maendeleo ya CDF vibaya ikiwa wana ushahidi wa kutosha.

“Mkishuku mbunge yeyote anazitumia pesa za umma vibaya mna ushaidi wa kutosha, heri mchukue hatua dhidi ya mshukiwa huyo kwa kuandaa kikao ili suluhu ipatikane. Hatutakubali pesa za maendeleo zitumike vibaya,” alisema Mbunge Moindi.

Wakati uo huo, Mbunge huyo aliomba wananchi kuunga mkono maendeleo yanayofanywa katika maeneo bunge yao kupitia pesa hizo za CDF ili maendeo yainuke zaidi katika Kaunti ya Kisii.

“Bila pesa za hazina hiyo hamna maendeleo yanawezafanyika katika sehemu za mashinani, kwa hiyo wakaazi wakiyaunga mkono maendeleo, Kenya yetu vile vile itainuka kimaendeleo,” aliongeza Moindi.

Kwa upande mwingine viongozi waliohudhuria hafla hiyo waliunga mkono pesa hizo kubaki kwa Serikali ya kitaifa na ziongezwe zaidi kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia 10.