Wenyeji wa Kaunti ya Kisumu wanatarajiwa kuadhinisha siku ya kimataifa ya matibabu ya sayansi ya kimaabara (International biomedical laboratory scientists' day) siku ya Ijumaa.
Sherehe hizo zitaandaliwa katika ukumbi wa michezo wa Jomo Kenyatta jijini Kisumu.
Akizungumza na wanahabari jijini Kisumu, mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Kisumu Elizabeth Ogaja alisema kuwa wataalamu mbali mbali wa afya watapeana huduma za matibabu ya bure kwa magonjwa mbali mbali ikiwemo kisukari, malaria na uchunguzi wa magonjwa mengine.
Ogaja alisema kuwa visa vya watu kuugua ugonjwa wa malaria na kuambukizwa virusi vya ukimwi vimeripotiwa kuongezeka katika eneo la Nyanza kwa jumla.
Aidha, aliwataka wenyeji wa Kisumu kujitokeza kwa wingi ili kupata matibabu hayo ya bure.
Kauli mbiu ya hafla hiyo itayoandaliwa na maabara ya kimatibabu ya kitaifa, (Kenya Medical Laboratory) kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Kisumu ni ‘Usalama wa mgonjwa kwanza’.