Huku ulimwengu ukijitayarisha kuadhimisha siku ya maji duniani siku ya Jumanne, wakaazi katika Kaunti ya Kisumu wametahadharishwa dhidi ya kuchafua vyanzo vya maji hasaa mito, inayoelekeza maji Ziwani Victoria.
Akizungumza siku ya Jumatatu, Chifu wa Kolwa Magharibi, inayojumuisha mitaa ya Nyalenda na Manyatta, Bwana Otieno Kabisai, alisema ni jukumu la kila mmoja katika jamii kuzingatia mazingira safi ili kukuza kizazi kinachozingatia umuhimu wa maji safi.
Kabisai alilaani hatua ya baadhi ya wakaazi wa Kisumu walio na mazoea ya kujisaidia karibu na mito na Ziwa Victoria, na kuwataka wakaazi kuchukua jukumu la kushtumu tabia hiyo na zingine za kuharibu mazingira.
“Ni hali ya kusikitisha sana mtu kuamua kujisaidia kando ya mito na Ziwa Victoria bila kuzingatia mazingira,” alisema Kabisai.
Kabisai alisema kuwa wenye mazoea ya kuchafua mazingira watakabiliwa kwa mujibu wa sheria na kusisitiza kuwa hatua ya kuoga katika mito na Ziwani Victoria inahatarisha afya ya mwanadamu na kuwaweka katika hatari ya kuvamiwa na wanyama kama vile nyoka na mamba.