Wakaazi wa Kisumu wametahadharishwa dhidi ya kupeana pesa kwa maafisa wa polisi kwa kisingizio kwamba ni pesa za kununua mafuta wanapohitaji usaidizi wa polisi.
Kamanda wa polisi wa utawala katika Kaunti ya Kisumu Joseph Keitany, amesema kuwa kupeana pesa kwa polisi ni ukiukaji wa maadili.
Keitany alisema kuwa polisi wamepewa magari na wao hupewa mafuta ya kutosha ishara kwamba wananchi hawafai kutoa pesa zozote kwa polisi ili kupokea msaada kutoka kwa maafisa hao.
Kwenye kikao na waandishi wa habari jijini Kisumu siku ya Jumatano, Keitany aliwaonya maafisa wa polisi dhidi ya kuitisha pesa kutoka kwa wananchi.
“Sisi kama polisi wa utawala, polisi wa kawaida na maafisa wa CID, tumepewa magari ya kustosha pamoja na mafuta ya kutosha. Yeyote atakayeambiwa kwamba atoe pesa za mafuta ndio asaidiwe na polisi, anafaa kupiga ripoti kwetu haraka iwezekanavyo ili hatua mwafaka zichukuliwe,” alisema Keitany.
Akizungumzia swala la usalama, Keitany alisema kuwa polisi wameimarisha usalama katika Kaunti ya Kisumu hasa katika maeneo ya mipaka.
Aliwaagiza washukiwa wote wa uhalifu wajisalimishe kwa polisi au wabadilishe miendendo yao, la sivyo, wakabiliwe ipasavyo.