Wakaazi katika Kaunti ya Kisumu wameshauriwa kutibu na kuchemsha maji ili kujiepusha na maradhi yanayotokana na mazingira machafu kama vile kipindupindu na amoeba.
Akizungumza siku ya Jumanne, Dkt Elly Nyambok, ambaye ni afisa mshirikishi wa uchunguzi wa magonjwa katika Kaunti ya Kisumu alisema kuwa ni muhimu kwa kila mmoja katika jamii kutibu maji ya matumizi ya nyumbani yakiwemo ya kunywa, ya kuoga na hata ya kuosha vyombo.
Aidha, aliwahimiza wakaazi wa Kisumu kuhakikisha wanachemsha maji ya aina yoyote yakiwemo ya mifereji ili kuua viini kama vile amoeba, ambavyo haviwezi vikaangamizwa kwa dawa ya maji aina ya chlorine peke yake.
Alisisitiza kuwa viini hivyo vyaweza tu kuangamizwa kwa kuchemsha maji hadi yakatokota.
Aidha, aliwataka wakaazi wanaoishi katika maeneo ambako mito inapitia na wanaopakana na Ziwa Victoria kuhakikisha kuwa vyanzo hivyo vya maji vinasalia kuwa safi.