Wakaazi wa mitaa ya Kondele, Manyatta na Nyalenda jijini Kisumu walisherehekea siku ya maji duniani kwa kujitokeza kuusafisha mto Auji.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mto huo ni miongoni mwa mito kadhaa ambayo huelekeza maji Ziwani Victoria.

Akizungumza siku ya Jumanne alipowaongoza wananchi kwenye zoezi la kuusafisha mto huo, mwakilishi wa Wadi ya Manyatta Bi Nereah Okombo aliwataka raia wanaoishi karibu na mto Auji kukoma kutupa taka kwenye mto huo.

Okombo alisema kuwa hazina ya Wadi ya Manyatta B imetenga shilingi milioni moja za kufanikisha zoezi la kuusafisha na kuutunza mto Auji, pamoja na kupanda miti na bamboo kando ya mto huo.

“Hoja ipo kwenye bunge la Kaunti ya Kisumu na hivi karibuni hoja hiyo itakua mswada utakaounda sheria ya kuzuia utupaji wa taka katika mto Auji. Mto huu ni muhimu sana na lazima tushirikiane kuutunza, kuuhifahi na kuulinda,” alisema Okombo.

Alisema kuwa watakua wakijitokeza kuusafisha mto huo kila baada ya miezi mine.

Zoezi la kuusafisha mto huo liliandaliwa na Shirika la Umande Trust tawi la Kisumu, serikali ya Kaunti ya Kisumu pamoja na wadau wengine.

Mwakilishi wa Wadi ya Kondele Ibrahim Mboya na mwenzake wa Manyatta B James Mbogo, ambao pia walishiriki zoezi hilo, walionya kuwa wanaochafua mto Auji watakabiliwa vikali kisheria.