Watu wawili wameaga dunia katika eneo la Got Nyabondo Wilayani Kisumu Mashariki kaunti ya Kisumu, kutokana na ugonjwa wa kipindupindu.
Mshirikishi wa uchunguzi wa magonjwa katika serikali ya Kaunti ya Kisumu Dkt Elly Nyambok, alisema kuwa jumla ya watu kumi wameambukizwa ugonjwa huo katika jimbo la Kisumu.
Akizungumza siku ya Jumanne katika uwanja wa DC Kassagam wakati wa maadhimisho ya siku ya maji duniani, Nyambok alisema kuwa ugonjwa huo unaendelea kuenea katika Kaunti za Kisumu, Nandi na Vihiga na kuwataka wakaazi kudumisha usafi ili kudhibiti kuenea kwa maradhi hayo.
Aliwarai wananchi kunawa mikono baada ya kutoka msalani, kabla na baada ya kula, kuchemsha maji ya matumizi nyumbani na kukoma kula kwenye hafla za umma kama matanga, ili kuzuia kuambukizwa ugonjwa huo.
“Ugonjwa wa kipindupindu unaendelea kuenea katika kaunti yetu ya Kisumu na kaunti jirani za Vihiga na Nandi. Lazima tudumishe usafi ili kuzuia kusambaa zaidi kwa maradhi hayo,” alisema Nyambok.
Alisema kuwa watu wanaopika na kula chakula katika maeneo mbali mbali ikiwemo kando ya barabara, wanafaa kusitisha biashara hiyo hadi ugonjwa huo utakapodhibitiwa.