Mwenyekiti wa Tume ya IEBC Wafula Chebukati akimpa Rais Mteule Uhuru Kenyatta cheti chake cha ushindi. [Picha/ PSCU]
Baadhi ya wakaazi wa Kaunti ya Lamu wamepinga ushindi wa Rais Mteule Uhuru Kenyatta na kusema kuwa sharti uchaguzi mpya kufanyika kwa muda wa siku 90.Wakaazi hao wameutaja uchaguzi huo kama uliokumbwa na utata hasa baada ya Tume ya IEBC kukosa kutimiza matakwa ya mrengo wa NASA.Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu, Silvence Kilomi, mkaazi wa Lamu Mashariki alisema sharti kesi iwasilishwe katika Mahakama ya Juu ili ushindi huo uweze kufutiliwa mbali.“Heri kesi ipelekwe mahakamani tena ili haki ipatikane na uchaguzi mpya kufanyika mara moja,” alisema Kilomi.Kilomi alisema kuwa Tume ya IEBC ilikosa kuwajibika vyema katika kuhakikisha kunafanyika uchaguzi wa huru, haki na usawa.Alimshutumu mwenyekiti wa Tume ya IEBC Wafula Chebukati kwa kumtangaza Uhuru kama mshindi licha ya uchaguzi kutofanyika katika maeneo bunge 25.“Kuna maeneo bunge 25 ambayo hayakushiriki katika uchaguzi huo sasa itakuwa vipi mshindi ametangazwa licha ya wakaazi wa maeneo hayo kukosa kupiga kura?” aliuliza Kilomi.Kwa upande wake, Miriam Mwero alisema kuwa hatambui ushindi huo wa Rais Uhuru na kusema kuwa sharti uchaguzi mpya ufanyike baada ya siku 90.Mwero alisema iwapo Uhuru anajali demokrasia na maslahi ya nchi, sharti ajiuzulu ili kuzuia fujo na ghasia kushuhudiwa nchini.“Uhuru anastahili kujiuzulu ili taifa lisishuhudie machafuko kama ya mwaka 2007/ 2008,” alisema Mwero.Aboubakar Said alielezea kutofurahishwa na hatua ya IEBC kumtangaza Uhuru kama mshindi na kusema kuwa tume hiyo imepoteza imani kwa wananchi.Saidi amewataka makamishana wote wa IEBC kujiuzulu ili tume mpya kuchaguliwa kusimamia marudio ya uchaguzi baada ya siku 90.