Wakaazi katika eneo la Dimbwini wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kukarabati mabomba ya maji taka ili kuzuia mafuriko katika eneo hilo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Haya yanajiri baada ya mafuriko kushuhudiwa katika eneo la Likoni kufuatia mvua nzito ambayo imekuwa ikinyesha katika eneo hilo tangu siku ya Jumapili.

Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, wakaazi hao wa Likoni walisema kuwa hawana namna nyingine ya kuzuia maji ya mvua kutoingia katika nyumba zao.

Wakiongozwa na mzee wa mtaa Abdi Suleiman, wakaazi hao walisema kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa imewafeli kwenye awamu nyingi kwani hiyo si mara ya kwanza kwa eneo hilo kukumbwa na hali kama hiyo hususan nyakati za mvua kubwa.

Wakaazi hao walisema kuwa walijipata katika hali ngumu ya kukabiliana na mafuriko wakati wa mvua ya El Nino na kuongeza kuwa hali hiyo sio tofauti na hali ambayo wameanza kushuhudia.

“Barabara zimefurika na inatubidi kutafuta njia mbadala ili kuenda kazini,” alisema Suleiman.

Aidha, wakaazi hao wamelalamikia ongezo la visa vya uhalifu kwa kusema kuwa vijana wa eneo hilo wamechukua nafasi hiyo kutatiza usalama kwa kuwaibia watu ambao husimama kujikinga mvua katika majumba.