Wakaazi wa Likoni wametakiwa kutoa taarifa kuhusu mikasa pindi tu yanapotokea ili kutoa nafasi kwa maafisa wa kukabiliana na majanga kutoa huduma za msaada kwa wakati unaofaa.
Akizungumza siku ya Jumatatu afisini mwake, mkuu wa polisi eneo la Likoni Bwana Willy Simba alisema ni jambo la kusikitisha kuona wakaazi wakizidi kuathirika kutokana na kutotoa habari za majanga wakiwa wamechelewa.
Akitoa mfano wa hivi juzi ambapo familia moja ilikadiria hasara kubwa baada ya nyumba yao kuteketea, Simba alisema kuwa baadhi ya wakaazi walishuhudia kisa hicho pasi na kuchukua jukumu la kutoa taarifa.
Aliwakosoa wakaazi hao na kusema kuwa inaashiria kukosa kuwajibikia maslahi ya wenzao.
Aidha, amekashifu vikali tukio lililotekea juzi katika eneo la Kisauni ambapo mwanamume mmoja aliteketea kiasi cha kutoweza kutambulika.
Simba alisema iwapo wakaazi wa eneo hilo wangetoa habari kwa vyombo vya usalama, basi maafisa wa zimamoto wangewasilii na kujaribu kudhibiti mkasa huo ambao ulipelekea mwanamume huyo kupoteza maisha yake.
Aidha, alisema kuwa kuna haja ya baadhi ya mashirika yasiyo kuwa ya kijamii kuanza kutoa mafunzo ya namna ya kujikinga na majanga pindi tu yanapotokea.