Wakaazi wa Majengo Mapya, Likoni, wameitaka serikali kuwajengea kituo cha polisi katika eneo hilo kufuatia ongezeko la visa vya uhalifu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Abdalla Sudi, ambaye ni mzee wa mtaa, ameitaka serikali kukabiliana na majambazi hao ambao wamekuwa kero kwa wakaazi wa eneo hilo.

“Tunahitaji kituo cha polisi katika eneo hili ili visa hivi vya ujambazi vipungue,”' alisema Sudi.

Alisema kuwa majambazi hao wamekuwa wakiwavamia wakaazi kiholela kila uchao na kuwapora, huku wengine wakiachwa wakiuguza majeraha.

“Hakuna usalama wala amani kwani kila siku watu wanavamiwa kwa visu na panga na kubaki na majera,” alisema Sudi.

Alisema hatua hiyo itaimarisha usalama, ikizingatiwa kuwa eneo hilo lina idadi kubwa ya watu.

“Eneo hili lina idadi kubwa ya watu ndio maana tunahitaji usalama wa kutosha. Baadhi ya vijana wanaoishi humu wamo miongoni mwa majambazi sugu katika eneo hili,” alisema Sudi.

Sudi alisema kuwa juhudi za maafisa wa polisi kutoka Likoni kuimarisha usalama hazitoshi kwa kuwa vituo hivyo viko mbali na mtaa huo.

Ameiomba serikali kushughulikia swala hilo kwa haraka ili kuwahakikishia wakaazi wa maeneo hayo usalama wa kutosha hasa wakati huu ambapo uchaguzi unakaribia.

Haya yanajiri baada ya maafisa wa polisi eneo la Likoni kuwatia mbaroni vijana 14 waliokuwa wamejihami kwa visu na mapanga kwa lengo la kutekeleza uhalifu.