Wakaazi wa maeneo ya Naikuro, Ogango na Nyakongo wilayani Manga, Kaunti ya Nyamira, wamelalamikia ongezeko la visa vya wizi wa ng’ombe katika maeneo hayo.
Haya yanajiri baada ya mjane mmoja kuibiwa ng’ombe wake usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu.
Wakizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Nyakongo, wakaazi hao waliomba maafisa wa polisi kufanya msako na kushika doria nyakati za usiku ili kukabiliana na wezi wa ng’ombe ambao wameonekana kuongezeka katika eneo hilo.
“Sisi wakaazi wa maeneo haya tumesumbuliwa sana na wezi wa ng’ombe na hatuwezi kabiliana nao maana huwa wamejihami kwa silaha hatari. Tunaomba maafisa wa polisi kutusaidia kwa kuwatia mbaroni wezi hao,” alisema Victor Mecha, mkaazi.
Wakati huo huo, wakaazi hao walisema kuwa wajane ndio walioathirika sana na wizi huo ikilinganishwa na wakaazi wengine.
“Ingawa sisi wakaazi wengine tunahangaishwa na wezi hao, wajane ndio wanaonekana kulengwa sana na magenge hayo ya wezi. Tunaiomba serikali kuingilia kati na kutusaidia kutatua swala hili,” alisema Jane Moseti, mkaazi.