Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa eneo la Miritini, Kaunti ya Mombasa wamelalamikia ujenzi wa reli mpya ya kisasa unaoendeshwa katika eneo hilo, huku wakidai kwamba maisha yao yanazidi kuwa magumu.

Wakaazi hao walisema kuwa tangu ujenzi huo uanze hawajawahi kupewa fidia yoyote licha ya kwamba walipewa ahadi hiyo huku sehemu zao za kufanyia ukulima zikivurugwa pamoja na mimea yao kuharibiwa.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne, Abdalla Mohamed, mmoja wa wakaazi alidai kuwa kampuni inayofanya ujenzi huo imekuwa ikiwadanganya kila mara.

“Walikuja wakachukua idadi ya makaburi, mimea, pamoja na sehemu zilizoathirika na wakasema kuwa watatulipa lakini tunaona kazi ikiendelea bila kupewa taarifa yoyote,” alisema Mohamed.

Mohamed alisema wengi wa wakaazi hao hufanya shughuli ya ukulima kujipatia kipato cha kila siku, huku wengine wakifanya biashara ya uvuvi ambayo pia imeathirika kutoka na uchafu unaorushwa baharini wakati wa ujenzi huo.

Hata hivyo, Mohamed alidai kuwa kuna baadhi ya wakaazi ambao waliwasiliti wenzao kwa kukubali hongo wanayopewa na washirika wa mradi huo na hivyo kususia shughuli za kupigania haki yao.

Kwa sasa wakaazi hao wanaiataka serikali ya kaunti kuingilia kati na kuhakikisha kuwa wamepata haki yao ya kupewa fidia kwani wengi wao wameshindwa kundelea na shughuli zao za ukulima ambazo walikuwa wakitegemea.

Sehemu zilizoathirika zaidi ni mtaa wa Miritini Madukani, Kipeta Uso na Mipirani.

Wakaazi hao waliamua kuungana pamoja na kuanzisha mchakato wa kutembelea mashirika mbalimbali pamoja na viongozi wa kiserikali, kutafuta msaada.