Wakaazi wa Mombasa wameapa kumpigia kura Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho iwapo atakiwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumatatu, wakaazi hao walidai kuchoka kuwapigania kura viongozi kutoka maeneo mengine na kusema kuwa wakati umefika kwa kiongozi kutoka Pwani pia kuchukua uongozi wa nchi.

“Tangu Kenya ipate uhuru, kila msimu wa uchaguzi wawaniaji wa urais wanapiga kambi hapa kutafuta kura. Kwanini sisi tusiwe na mmoja wetu naye azuru maeneo mengine kuwarai wananchi kumpigia kura atawale nchi,” alisema Mzee Yusuf.

Aidha, wakaazi hao walipendekeza wabunge wapitishe mswada bungeni utakaowezesha wananchi kupiga kura ya maoni ili katiba ifanyiwe marekebisho kuhakikisha kuwa viongozi kutoka sehemu moja hawaruhusiwi kuwania kiti cha urais ikifuatana.

“Hii katiba yetu inafaa ifanyiwe mageuzi. Haiwezikani watu wa ukoo mmoja kuongoza nchi kila mara huku wengine wakisalia wapiga kura kila msimu,” alisema Mama Fatuma.

Akizungumza siku ya Jumapili katika msururu wa mkutano na wakaazi wa Mombasa, Gavana Hassan Joho alitangaza azma yake ya kutaka kukiwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.