Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki amesema kuwa polisi wameweka mikakati kabambe ya kuimarisha usalama mwezi huu wa Disemba.
Akizungumza katika kikao na wanahabari jijini Mombasa, Achoki alisema kuwa maafisa wa vitengo mbali mbali tayari wamegawanywa katika maeneo tofauti ya burudani ili kuhakikisha kuwa shamra shamra za mwezi huu wa Disemba hazitatatizwi.
“Mikakati maalum imewekwa na idara ya usalama ili kuhakikisha kuwa likizo kwa wakaazi wa Mombasa na wageni kutoka maeneo mbali mbali inafana,” alisema Achoki.
Aidha, alisema kuwa idadi ya maafisa wa usalama imeongezwa katika maeneo ya burudani, Uwanja wa ndege wa Moi, bustani mbalimbali na fuo za bahari ili kukabiliana na yeyote yule atakayenuia kuleta vurugu wakati wa sherehe hizi za mwisho wa mwaka.
Vile vile, alisema wamezindua aina maalum ya king’ora kitakachotumika na wakaazi kuwajulisha maafisa wa usalama kuhusu visa vyovyote vya uhalifu.
Hata hivyo, kamishna huyo amewataka maafisa wa usalama kuwajibikia majukumu yao vyema bila kuwanyanyasa au kuwadhulumu wananchi.
“Maafisa wa usalama tambueni kuwa jukumu lenu ni kuwalinda wananchi na sio kuwahangaisha au kuwanyanyasa wakati wa operasheni zenu,” alisema Achoki.
Kamishna huyo amevitaka vitengo vya usalama vya kiserikali na vile vya kibinafsi kushirikiana ili kufanikisha zoezi hilo la kuimarisha usalama.