Wakaazi katika kaunti ya Mombasa wameonya dhidi ya kupotoshwa na baadhi ya wanasiasa wanaolenga kuwagonganisa kuhusu mpango wa serikali ya kaunti wa kuzibomoa nyumba kuu kuu katika kaunti hiyo.
Mkuu wa Idara ya Ardhi, Makao na Mipangilio ya Mji katika Kaunti ya Mombasa Antony Njaramba amesema kuwa baadhi ya wanasiasa wanawachochea wakaazi wanaoishi katika nyumba zinazolengwa kubomolewa ili kupinga mradi huo, licha ya kaunti ya Mombasa kutaka kuboresha mji wa Mombasa.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Njaramba alisema kuwa wanasiasa hao wana uwezo wa kujenga nyumba za kifahari lakini uchochezi waouendeleza ni kwa kuwa wanahofia kuingia hasara.
Njaramba alisema kuwa mpango wa Kaunti ya Mombasa ni kuboresha hali ya maisha ya wakaazi.
"Tunawaambia wanasiasa kukoma kuwagonanisha wakaazi wa Mombasa kutokana na mradi tunaolenga kuanzisha wa kuboresha mji wa Mombasa kwa kuzibomoa zile nyumba kuu kuu. Wanapinga mradi huo kwa kuwa wanajua watakosa wateja kwasababu nyumba tunazonuia kujenga zitakua nzuri na rahisi kwa wakaazi wetu,” alisema Njaramba.
Mpango huo unalenga kuzibomoa nyumba za wakaazi wa eneo la Buxton, Tudor, Likoni, na Makande zinazomilikiwa na serikali ya kaunti, na kuzijenga upya ili kuboresha kaunti ya Mombasa.