Viongozi katika Kaunti ya Mombasa wakiwemo wa serikali, wa kidini na wa mashirika zisizo za serikali wameanzisha kampeni ya kuhakikisha kuwa vijana waliojisajili ili kupata vitambulisho wamezichukua pindi zinapotoka.
Akizungumza siku ya Jumatatu, afisa aneyesimamia shuguli ya kupata vitambulisho katika Kaunti ya Mombasa Aggrey Maasai, alisema kuwa vijana hao hukawia sana kabla ya kuchukua stakabadhi hizo.
Maasai alisema kuwa kitambulisho ni muhimu kwani stakabadhi hiyo ndiyo inayomwezesha mtu kupata fursa nyingi za kikazi na hata kumwezesha kupata mkopo katika benki ili kutekeleza miradi tofauti ya kujiendeleza.
Aidha, alisema kuwa zaidi ya vitambulisho elfu 20 havijachukuliwa kutoka katika kituo cha Huduma Centre Kaunti ya Mombasa, huku akiongeza kuwa huenda tarakimu hizo zikaongezeka wakati unavyosonga.