Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa imetoa tahadhari kwa wakaazi kuzingatia usafi wa mazingira na maji ya matumizi ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa homanyongo (A).
Akizungumza kwenye kikao na waandishi wa habari afisini mwake siku ya Jumanne, mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa, Mohammed Abdi, alisema kuwa huenda ugonjwa huo ukasambaa iwapo wakaazi hawataimarisha hali yao ya usafi.
Aidha, Abdi alithibitisha kuripotiwa kwa visa 21 vya ugonjwa huo katika hospitali za kibinafsi wiki iliyopita mjini humo.
Hatahivyo, aliondoa hofu kwa wananchi kwa kutoa hakikisho kuwa serikali ya kaunti tayari imeweka mikakati dhabiti ya kuukabili ugonjwa huo.
“Kama serikali ya kaunti tutafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa wananchi wetu wako salama. Tayari tumeafikiana na kampunzi za kusambaza maji kuhakikisha kuwa maji yanatiwa dawa kabla kusambazwa kwa matumizi,” alisema Abdi.
Waziri huyo vilevile alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa imeweka uangalizi mkali wa kiafya katika mipaka yake na kaunti zingine ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa homa ya manjano ulioripotiwa kuzuka mjini Nairobi wiki iliyopita.