Baada ya siku kadhaa za joto kali na kumwaga jasho jingi kwa wakaazi wengi wa maeneo ya Pwani, wenyeji mwishowe wamepata nafuu ya muda kufuatia mvua iliyonyesha siku ya Jumanne na kupunguza makali ya miale ya jua.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mvua hiyo ambayo ilinyesha katika maneo ya Kaunti ya Mombasa kuanzia usiku wa manane ilileta uangavu na nusura kuu miongoni mwa wenyeji wa kaunti hiyo ambao kwa zaidi ya miezi mitatu wamekuwa wakilalamikia uwepo wa joto kali.

Akiongea na mwandishi huyu mjini Mombasa, Salmah Ousman, mkaazi katika eneo la Kibokoni, alisema kuwa kwa muda huo wote ilikuwa vigumu kwake kutembea hata nusu kilomita kwa sababu ya kuchomwa mno na jua.

Alisema kuwa hali hiyo ilimfanya kutumia fedha nyingi kwa vile alikuwa akilazimika kutumia tuktuk kuwapeleka watoto wake shuleni.

“Tunamshukuru Mola kwa vile angalau sasa tunaweza kutembea hadi shuleni na wanangu bila kutumia bodaboda wala tuktuk. Naomba mvua hii iendelea kunyesha angalau hali ya anga iweze kuleta nafuu upande wa joto,” alisema Ousman.

Susan Mwasighe, ambaye ni mkazi wa eneo la Bouxton jijini Mombasa, alisema kuwa amehisi tofauti baada ya kunyesha kwa mvua hiyo nzito asubuhi ya siku ya Jumanne na kutoa matumaini kuwa joto hilo litapungua.

Hata hivyo, wengi walihisi kuwa nafuu hiyo ni ya muda kwani si mara ya kwanza joto kushuhudiwa kwa viwango kama hivyo katika eneo la Pwani, na kusema mvua hiyo ni ya muda na joto litarudi ilivyo kawaida.