Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Mombasa limezindua mpango wa kusambaza dawa za kutibu maji kwa wakaazi wa Kaunti hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mkuu wa Shirika hilo katika Kaunti ya Mombasa Mohammed Rajab, amesema kuwa tayari visa 21 vya ugonjwa wa homanyongo (A) vimethibitishwa na Idara ya afya katika kaunti hiyo na ni lazima mikakati ya dharura kuzinduliwa ili kuhakikisha kwamba ugonjwa huo unadhibitiwa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Rajab alikiri kwamba mkurupuko wa homanyogo umechangiwa na maji chafu ambayo wakaazi wamekuwa wakitumia na kuipa changamoto serikali ya Kaunti ya Mombasa kuhakikisha maji yanayosambazwa kwa wakaazi wa kaunti hiyo ni safi.

Afisa huyo alisema kwamba kadri msimu wa mvua unavyokaribia, shirika hilo litaendelea kusambaza dawa za kutibu maji na kuwashauri wakaazi wa kuanti hiyo kuzingatia usafi wa mazingira ili kujikinga na mkurupuko wa maradhi.

"Tayari tumeanza mikakati ya kutibu maji katika Kaunti ya Mombasa hata yale ya visimi ili kuzuia kushuhudiwa kwa mkurupuko ya maradhi hasa msimu huu wa mvua, ikizingatiwa kuwa baadhi ya visima huchafuka kutokana na mazingira duni,” alisema Rajab.

Afisa huyo aliyataja maeneo ya vitongoji duni kama vile Moroto na Mburu Kenge katika eneo la Tudor na Bangladesh huko Jomvu, kama baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia mkurupuko wa maradhi pindi mvua inaponyesha.