Kiongozi wa NASA Raila Odinga akiapishwa kama rais wa wananchi. /AFP
Maelfu ya wafuasi wa NASA Kutoka kaunti ya Mombasa walikaribisha uapisho wa kinara wa NASA Raila Odinga kwa hisia tofauti.
Wengi wa wafuasi wa NASA walisema kuwa viongozi wengine wa muungano huo kama Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wanahitaji kutoa sababu za ni kwa nini hawakuwepo katika bustani ya Uhuru mjini Nairobi.
“Lazima viongozi wengine ambao hawakuwa Uhuru park watueleze mbona hawakufika,’’ Walisikika wakisema.
Hata hivyo kinara wa NASA Raila Odinga alisema kuwa wenzake hawakuweza kufika katika bustani ya Uhuru kwa sababu ambazo zitatajwa baadaye.
Baadhi ya wakaazi wa mji wa wa Mombasa walisema kuwa gavana wa Mombasa Hassan Joho anahitaji kumridhi Kalonzo Musyoka kama naibu kiongozi wa NASA.
Wengi wa wakaazi walisema kuwa hatua ya kuapishwa kwa Raila Odinga imewapatia matumaini makubwa sana na kwao.
“Kwetu sasa taifa la Kenya limezaliwa upya na nina imani Raila atahakikisha kuwa maswala mengi yatashughulikiwa,’’ alisema Rashid mmoja wa wakaazi wa Mombasa.
Mapema leo naibu gavana wa Mombasa William Kingi alisema kuwa ni ilikuwa ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu kwa mamlaka ya mawasiliano nchini CAK kwa kufunga runinga ambazo zilikuwa zikipeperusha matangazo ya moja kwa moja kutoka bustani ya Uhuru.