Wakaazi wa Mombasa wameeleza kughadhabishwa na hatua ya wabunge wa kaunti hiyo kuviahirisha vikao vya bunge vya siku ya Alhamisi ili kumsindikiza Gavana Hassan Joho kuandikisha taarifa kwa idara ya usalama mjini Malindi.
Wakizungumza na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Alhamisi, wakaazi hao walitaja hatua hiyo kama inayoashiria namna viongozi wa kisiasa nchini wanavyoweka mbele maslahi yao ya kibinafsi badala ya kuwahudumia wananchi waliowapigia kura.
‘’Kama wakaazi wa Mombasa tunamuunga mkono gavana wetu katika juhudi zake lakini hiyo haimanishi kuwa anaweza fanya shughuli zote za kaunti zisimame. Mtu mmoja hawezi sababisha baishara ya kaunti nzima kusitishwa,’’ alisema mkaazi mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa.
Wakaazi hao sasa wamewataka wabunge hao wa kaunti kukoma kujihusisha na masuala yasiyowafaidi wenyeji na badala yake kutekeleza miradi ya maendeleo yatakayochangia kuinua hali ya maisha ya watu wenye mapato ya chini.
Vikao vya bunge la Mombasa vilikosa kuendelea kama kawaida siku ya Alhamisi, baada ya wabunge wa kaunti kuandamana na Gavana Hassan Joho hadi kituo cha polisi mjini Malindi kuandikisha taarifa kuhusiana na vurugu zilizoshuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi mnamo Machi 7.