Idara ya usajili wa watu katika Kaunti ya Mombasa imewataka wakaazi waliojiandikisha kupata vitambulisho kuchukua stakabadhi hizo kutoka kwa ofisi husika.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mtendaji wa usajili wa vitambulisho eneo la Kisiwani Mombasa, Naomi Birya, amewataka wazee wa mitaa kuchukua jukumu la kuwahimiza wakaazi kwenda kuchukua vitambulisho vyao.

Akizungumza siku ya Alhamisi, Bi Birya alisema kuwa kuna zaidi ya vitambulisho 6,000 katika ofisi zao ambavyo bado havijachukuliwa na wenyewe.

Afisa huyo alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakifungiwa nje ya miradi mbalimbali ya maendeleo na hata kukosa ajira kwa sababu ya kukosa vitambulisho.

Aidha, aliwataka wote ambao wamefikisha umri wa kupata vitambulisho kufika katika ofisi za usajili wa vitambulisho ili kusajiliwa.