Wakazi wa Kaunti ya Mombasa wamehimizwa washirikiane na Maafisa wa Afya wa Kaunti hiyo ili kufanikisha kampeni za utoaji chanjo za maradhi ya ukambi na pepopunda zitakazoanza Jumatatu wiki ijayo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika kongamano la kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa chanjo hizo mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Afisa Mkuu wa Afya katika Kaunti hiyo Daktari Khadija Shikely, alisema kuwa chanjo hizo zinasaidia kukinga maradhi.

Aidha, afisa huyo wa afya alipuuzilia mbali kauli za baadhi ya viongozi wa dini wanaodai kuwa chanjo hizo ni za kupanga uzazi, akisema hizo ni kasumba tu.

“Tunawahimiza wakaazi kuhakikisha kuwa wanazingatia maagiza ya wataalum wa kiafya kuhusu umuhimu wa chanjo hii na kuepukana na tuhuma za baadhi ya watu kuwa tuko na lengo la kuwapa wanawake na chanjo za kupanga uzazi”,alisema Daktari Shikely.

Kwa upande wake Baraza la Maimamu na Wahubiri wa humu nchini Kaunti ya Mombasa limewahimiza wazazi wawapeleke watoto wao katika vituo vya afya ili wapate chanjo hizo.