Shirika la Msalaba Mwekundu limetoa tahadhari ya mafuriko katika Kaunti ya Mombasa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, afisa mkuu wa shirika hilo Mohammed Rajab aliwataka wakaazi kuwa waangalifu msimu huu wa mvua.

"Tunawaomba wakaazi kuwa makini sana hasa wakati huu wa msimu wa mvua ili kuepukana na maafa na majanga,” alisema Rajab.

Haya yanajiri baada ya zaidi ya familia 100 kuathirika na mafuriko huko Bangladesh, eneo bunge la Jomvu.

Familia hizo zimenufaika na msaada kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Mombasa.

Shirika hilo liliwafadhili waathiriwa hao mahema, vyandarua vya kuzuia mbu pamoja na vyombo vya kutumia.

Rajab alisema kuwa shirika hilo kwa sasa linashirikiana na serikali ya Kaunti ya Mombasa ili kuona kuwa waathiriwa hao wanaregelea hali yao ya kawaida ya maisha licha ya nyumba zao kubomolewa kufuatia mafuriko.

Afisa huyo aidha alisema kuwa maafisa wa afya pia watawahudumia waathiriwa hao ili kuzuia mkurupuko wa maradhi hasa kwa watoto wadogo.