Mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa amewataka wakaazi kuzingatia usafi kwa kuyaondoa maji yaliyotuama kwenye vidimbwi.
Akizungumza afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mohammed Abdi alisema kuwa hatua hiyo itawasaidia wakaazi kujikinga dhidi ya maradhi kama vile malaria, ambayo maambukizi yake huongezeka wakati wa mvua kubwa.
Abdi alisema kuwa msimu huu wa mvua huenda ukaambatana na magonjwa yanayotokana na kutozingatia hali ya usafi hususan wa maji.
“Wakaazi wanapaswa kuanza kuchukua jukumu la kutengeneza njia za maji yaliyo kwenye vidimbwi. Hatua hiyo itawasaidia kujikinga kutokana na mbu,” alisema Abdi.
Abdi aidha alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa itashirikiana na wazee wa mitaa kuhakikisha kuwa wanasambaza dawa za kunyunyiza katika vidimbwi ili kuzuia mbu.
Mkuu huyo wa idara ya afya alisema kuwa huenda maradhi ya malaria na kipindupindu yakaanza kushuhudiwa ikiwa wakaazi hawatatilia maanani umuhimu wa usafi.
Aidha, ametoa wito kwa wakaazi wa Changamwe ambako magonjwa hayo huripotiwa zaidi kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanaishi katika mazingira safi.