Mwanamme mmoja mwenye umri wa makamu alijitoa uhai Jumatatu jioni saa chache baada ya kutoka katika handaki moja la pombe haramu katika eneo la Mukinyai Molo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kulingana na familia, Rufus Ndirangu baba wa watoto watatu, aliingia chumbani mwake saa nne unusu usiku akionekana mwenye hasira na kuelekea katika chumba chake cha kulala.

Walipoamka Jumanne asubuhi walimpata kama amejitia kitanzi.

Kisa hicho kilisababisha maandamano ya wakaazi wakishtumu uongozi tepetevu wa polisi eneo hilo, kwa madai kwamba wanashirikiana na wapishi wa pombe haramu kuendeleza biashara hiyo.

Mkaazi Simon Wanyoike alisema: “Zaidi ya vijana wanne wameaga dunia katika kipindi cha miezi sita kutokana na pombe haramu.”

 Wakaazi wamemtaka katibu katika wizara ya ndani Karanja Kibicho kuwachukulia hatua maafisa wa usalama eneo hilo kama anavyofanya kwingineko

Wakaazi hao waliojawa na hamaki baadaye walivamia vituo vya kuuzia pombe haramu katika eneo la Migaa, Sachangwan, Kianugu, Mukinyai na Gitinge ambapo waliharibu pombe.