Baada ya kambi ya matibabu ya bure kuandaliwa siku mbili zilizopita katika Shule ya msingi ya Tudor, zoezi hilo linatarajiwa kurejelewa kufuatia lalama kutoka kwa wakaazi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amesema kuwa hatua hiyo imeafikiwa baada ya kubainika kuwa kulikuwa na uhaba wa vifaa vya kuwapima wakaazi maradhi mbalimbali, huku akiongeza kuwa zoezi hilo litarejelewa siku ya Jumatatu.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Nassir alisema kuwa hali hiyo inaashiria wazi kuwa wakaazi wameingiwa na hofu kufuatia mkurupuko wa ugonjwa wa homanyongo A, na lazima hatua mwafaka zichukuliwe ili kuhakikisha wakaazi wa eneo bunge la Mvita hawaathiriwi na maradhi hayo.

“Tumeamua kuzindua mpango huu ili kuwasaidia wakaazi wa eneo bunge la Mvita na Mombasa kwa jumla, kupata matibabu ya bure yasiokuwa na malipo ili kudhibiti kuchipuka kwa maradhi ya kiafya,” alisema Nassir.

Mbunge huyo aliwahimiza wakaazi kujitokeza siku ya Jumatatu ili kunufaika na kambi hiyo ya matibabu ya bure kwa lengo la kukabili ugonjwa wa homanyongo A na maradhi mengine ya kiafya.

Kauli ya Nassir inajiri huku Idara ya Afya Kaunti ya Mombasa ikipambana na zaidi ya visa 120 vya ugonjwa huo wa homanyongo katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita.