Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amewahimiza wakaazi wa eneo bunge lake kuwajibikia miradi iliyoanzishwa eneo hilo chini ya usimamizi wa afisi yake ili kujisaidia maishani.
Akzingumza na kamati ya usimamizi wa miradi hiyo, Nassir amewaomba wanakamati wote kujitwika jukumu la kuwahamasisha wananchi kuhusu manufaa ya miradi hiyo, huku akiwataka wenyeji pia kuzingatia umuhimu wa miradi hiyo maishani.
Kamati ya miradi ya maendeleo eneo bunge la Mvita chini ya usimamizi wa mbunge Nassir ilibuni na kuanzisha miradi ya Green House, mabwawa ya samaki, maktaba kwa wanafunzi, kuanzishwa kwa Shule ya upili ya Mvita Stima pamoja na maabara ya Serani, lengo kuu likiwa kuinua viwango wa maisha ya wenyeji wa Mvita.
Aidha, mbunge huyo ambaye ameondoka humu nchini kueleka nchini Marekani kuhudhuria kongamano la kitaifa la wabunge nchini humo, litakaloandaliwa kati ya tarehe saba na kumi na moja mwezi Agosti, ametoa wito kwa wakaazi wa Mvita kukumbatia miradi hiyo, huku akiwarai wanafunzi kutumia maktaba hiyo kila wakati ili kuinua viwango vya elimu.
Wenyeji wa eneo hilo wamesema maabara hiyo itasaidia kutambua hali yao ya kiafya ili kuhakikisha kwamba jamii iko salama kiafya.
Mbunge huyo anatarajiwa kurejea humu nchini punde tu kongamano hilo litakapokamilika.