Shirika la wanyamapori nchini, KWS, sasa limetakiwa kujenga ua ili kuwazuia viboko kutowahangaisha wakaazi wa eneo la Mwariki viungani mwa mji wa Nakuru.
Wakaazi hao waliozungumza na mwandishi huyu Alhamisi walisema viboko hao wanaoishi katika vidimbwi vya maji taka kwenye eneo hilo wamekuwa tishio kwa usalama wao.
Aidha, walisema malalamishi yao ya mara kwa mara kwa shirika hilo, hayafua dafu kwani hawajapata usaidizi wowote.
‘Watu huwa wanalalama kwa KWS kuhusu viboko hao lakini hakuna hatua ambazo zimechukuliwa hadi sasa. Tunataka waondolewe,’ alisema Jane Njeri.
Walisema viboko hao wamekuwa wakihangaisha watoto wao hasua wanapocheza.
‘Wakati mwingine kiboko hutoka katika kidimbwi cha maji watoto wetu wanapocheza na kuwakimbiza. Viboko hao huwa wanatokea nyakati za jioni,’ aliongezea Alice Waceke.
Wengine wao sasa wanashauri shirika hilo kuweka ua la kuwazuia viboko hao kufika karibu na makaazi yao.
‘ Tunataka waweke ua. Wakati mwingine hata fisi huja katika makaazi yetu nyakati za usiku. Kuna wakati mmoja ambapo fisi walikula mbuzi wa mama mmoja hapa . Tunahofia fisi hao wataumiza pia watoto wetu,’ alisema Joseph Kinuthia.
Juhudi za kuzungumza na maafisa wa KWS kuhusiana na swala hilo hazikufua dafu kwani hawakupokea simu walizopigiwa.