Wakaazi wa vijiji vya JC, Kiamaina na Kiugu katika wadi ya Kabatini, waliandamana Ijumaa asubuhi kutokana na kukidhiri kwa swala ka pombe haramu, ambapo kijana mwenye umri wa miaka 23 Charles Macharia alifariki asubuhi hiyo kutokana na utumizi wa pombe haramu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Zaidi ya wakaazi 300 waliokuwa wamebeba matawi, walifanya maandamano ya amani kutoka kituo cha kibiashara cha JC hadi kwenye kituo cha polisi cha Kiugu, kulalamikia polisi kukosa kuchukua hatua madhubuti za kumaliza pombe.

Wakaazi hao walilaumu kituo hicho cha polisi chini ya usimamizi wa OCPD Duncan Nguthu, wakisema walikataa kwenda kuuchukua mwili wa mwendazake kwa madai kwamba gari lao halikuwa na mafuta.

“Sisi tumewajulisha polisi kuhusu kifo cha kijana huyu ambaye amekuwa mraibu wa pombe, lakini wakasema tujichukulie mwili kwa sababu gari lao halina mafuta. Kazi yao imekuwa ni kuhangaisha vijana wa boda boda na watu wa karakana, lakini hawamalizi pombe kwa sababu wanahongwa,” akasema Munyiri wa Mbarire mkaazi.

Nduguye marehemu kwa jina Steven kamangai, alisema polisi hao huchukua hongo ya shilingi 2,000 kutoka kwa kila handaki la chang’aa.

Marehemu Charles Macharia alipatikana maiti kwenye mtaro asubuhi ya Ijumaa, huku wakaazi wakisema alifariki baada ya kulewa pombe haramu kupita kiasi Alhamisi usiku.

OCPD Duncan Nguthu alikataa kuzungumzia swala hilo, akisema kwamba amo harakatini za kuandaa mkutano wa maombi ya shukrani kwenye uwanja wa Afraha, utakaohudhuriwa na rais Kenyatta.

Naye OCS wa Bahati David Rono aliyekuweko kwenye kituo hicho, alisema hana mamlaka ya kuzungumiza swala hilo “kwa sababu OCPD hajanipa idhini”.