Baadhi ya wakaazi wa eneo bunge la Nyali wamepongeza hatua ya Mwakilishi wa Wadi ya Kongowea Jabes Oduor, yakutaka kupunguzwa kwa mshahara wake kwa asilimia 50.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumatatu, wakaazi hao, wakiongozwa na Otieno Odour, walisema kuwa hatua hiyo ni ya busara na kumtaja mwakilishi huyo kama mwenye busara.
Wakaazi hao walisema kuwa pesa hizo zinafaa kutumika vyema kwa kuwasaidia mayatima hao.
“Viongozi wengine wanafaa kuiga mfano wa mwakilishi wadi huyo na kurudisha shukrani kwa wananchi waliowachagua,” alisema Oduor.
Itakumbukwa kuwa Mwakilishi wa Wadi ya Kongowea Jabes Oduor, alimuandikia barua Spika wa Bunge la Kaunti ya Mombasa Thadius Rajwayi, akitaka mshahara wake upunguzwe kwa asilimia 50 kuanzia mwezi Mei mwaka huu.
Katika barua hiyo iliyotumwa kwa wanawahabari siku ya Jumamosi, Oduor alisema anataka mshahara wake upunguzwe sambamba na marupurupu yake katika kipindi kilichosalia kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Barua hiyo ilieleza kuwa Oduor alichukua hatua hiyo ili kuwasaidia watoto mayatima katika makaazi ya Angaza Children Centre katika eneo bunge la Nyali.
Spika wa bunge hilo Thadius Rajwayi, alikiri kupokea barua hiyo na kuthibitisha kuwa matakwa ya Oduor yatazingatiwa.