Wakaazi katika kanda ya Pwani hususan eneo la Ngomeni, katika kaunti ndogo ya Magarini, wametakiwa kutoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu na ugaidi kwa maafisa wa usalama ili washukiwa hao waweze kutiwa nguvuni.
Akizungumza siku ya Ijumaa, afisa msimamizi wa kitengo cha polisi wa utawala wanaoshika doria katika maeneo ya mipakani Meshack Mwalo, amesema kuwa kikosi hicho kinalenga kuhakikisha kuwa washukiwa wa ugaidi wanakamatwa.
Mwalo aliwahakikishia wakaazi wa eneo hilo usalama dhabiti, kwa kusema kuwa serikali kupitia vitengo tofauti vya usalama viko macho kuhakikisha kuwa wakaazi wanaisha bila hofu.
Afisa huyo aliongeza kuwa tayari serikali imepata habari muhimu kuhusiana na washukiwa wa ugaidi ambao lengo lao kuu ni kutatiza amani katika eneo hilo ambalo linapakana na bahari hindi.
“Tunawaomba wakaazi kushirikiana na polisi katika kutoa habari muhimu kuhusu washukiwa wa ugaidi na wahalifu ili waweze kutiwa nguvuni. Tunawahakikisha wakaazi usalama dhabati na wala wasiwe na hofu,” alisema Mwalo.
Aidha, alisema kuwa maeneo ya Ngomeni, Cheshale, Mambrui miongoni mwa maeneo mengine yanayopakana na bahari hindi tayari yamepewa usalama.