Wakaazi katika eneo la Pwani wamehimizwa kuboresha uhusiano mwema baina yao na maafisa wa usalama kama njia moja ya kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kijamii la Kenya Community Support Centre KECOSCE, Phyllis Muema, amesema kuwa tayari ameanzisha hamasisho kwa jamii kuhafamu umuhimu wa kuboresha uhusiano mwema na maafisa wa salama.

Akizungumza katika eneo la Likoni mjini Mombasa siku ya Jumanne katika kongamano la amani, Muema alisema kuwa iwapo juhudi hizo zitafaulu, basi maswala ya uhalifu, ugaidi na misimamo mikali itapungua kwa kiasi kikubwa.

Muema alisema kuwa shirika hilo litahakikisha kuwa juhudi za kuboresha uhusiano mwema baina ya jamii na maafisa wa usalama zinaimarishwa ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa njia ya amani.

“Tunawahimiza wakaazi wa eneo hili kuhakikisha kuwa wanakabiliana vilivyo na utovu wa usalama kwa kuboresha uhusiano mwema baina yao na polisi. Hatua hiyo itatuwezesha kukabiliana na uhalifu,” alisema Muema.

Shirika hilo kwa sasa linaendeleza zoezi la kuwahamasisha wakaazi kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na usalama kwa kushirikiana na maafisa wa polisi.