Maafisa wa mazingira wamewataka wakaazi wa Pwani kujukumika na kupanda miti aina mbalimbali msimu huu wa mvua za masika, ili kudhibiti mabadiliko ya hali ya anga yanayoikumba sehemu hiyo kila mara.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kulingana na Arafa Abdallah, ambaye ni mwanasayansi katika taasisi ya utafiti wa misitu nchini, al maarufu’ Kenya Forestry Institute’ (KeFRI) katika kitengo cha upandaji wa miti, ongezeko la mahitaji ya ardhi katika eneo la Pwani limechangia pakubwa kukatwa kwa misitu kwa kuwa idadi ya watu inaongezeka.

Hata hivyo, alisema kuwa jambo la kushangaza ni kuwa miti hiyo inapokatwa, hakuna hata mmoja anayejitolea kupanda mti mwingine.

Akizungumza kwenye warsha iliyowaleta pamoja wakaazi na wakulima kutoka kaunti ndogo ya Rabai, Arafa alisema kuwa eneo la Pwani limekuwa likikumbwa na ukataji miti kwa wingi kutokana na biashara ya makaa.

"Biashara hiyo imechangia pakubwa ongezeko la ukosefu wa mvua sehemu za Pwani ambako familia nyingi haswa kutoka mashinani hukumbwa na uhaba wa chakula kutokana na ukosefu wa mvua ya kutosha, inayohitajika kwenye upanzi wa mimea ya vyakula," alisema Arafa.

Arafa aidha alisisitiza umuhimu wa kupandwa kwa miti na kuongeza kuwa endapo wakaazi watakumbatia wito huo, basi eneo la Pwani litakuwa likipata mvua na kupunguza viwango vya joto.

Kwa upande wake, Leila Ndalilo, mwanasayansi katika taasisi ya misitu alisema ni muhimu kwa jamii za Pwani kufuatilia njia za kuhifadhi mazingira walizofundishwa kwenye warsha hiyo pamoja na kukumbatia teknolojia ya kisasa katika kuboresha hali ya mazingira.

Aidha, alisema kuwa tayari taasisi ya misitu pamoja na Idara za Mazingira katika kaunti za Pwani zimeafikiana namna ya kuanzisha miradi ya kupanda miti haswa wakati huu ambapo mvua za masika zinapoendelea kushuhudiwa kote nchini.