Kiongozi wa dini ya kikatoliki jijini Mombasa Martin Kivuva ametoa wito kwa wakaazi wa ukanda wa Pwani kutowaua wazee kwa tuhma za uchawi.
Akiongea katika Kanisa la Barnaba lililopo eneo la Kaloleni, kiongozi huo alilaani kitendo cha kuwahusisha wazee na uchawi kwa sababu ya kuwa na nywele nyeupe wanapozeeka.
Kivuva alitaja kasumba ya kuhusisha nywele nyeupe na uchawi kama potovu.
Aidha, alisisitiza kuwa nywele nyeupe ni dalili ya hekima na kuongeza kuwa kitendo hicho ni cha kinyama na hakikubaliki hata katika tamaduni za kiafrika.
Kiongozi huyo aliwataka wanasiasa kutoka eneo hilo kuwajibika na kukabili swala hilo tata kwa kuhubiri amani.
Pia aliwataka vijana wanaodaiwa kujihusisha na vitendo hivyo kujiepusha navyo na badala yake kuwajibika katika ujenzi wa taifa.
Mauaji ya wazee kwa tuhma za uchawi katika ukanda wa Pwani yamekithiri, huku vijana wadogo wakidaiwa kujihusisha na vitendo hivyo.
Inaripotiwa kuwa baadhi ya wazee wakongokwe wamelazimika kuhama makwao baada ya kupokea vitisho.