Tahadhari imetolewa kwa madaktari na wakaazi wa ukanda wa Pwani kuhusu kuzuka kwa ugonjwa wa Chikunguya.
Katibu mkuu katika Wizara ya Afya Dr Nicholas Muraguri amesema ingawa ugonjwa huo sio hatari, wizara hiyo imetoa tahadhari kwa madaktari katika Kaunti za Mombasa, Lamu, Garissa na kaunti zilizopo katika eneo la mwambao wa Pwani kuhusu kuzuka kwa ugonjwa huo.
Alisisitiza kuripotiwa kwa visa vya ugonjwa huo kwa wataalam iwapo utazuka ili hatau za haraka za matibabu kuchukuliwa.
Hali hiyo imetokea huku serikali ikipeleka dawa za thamani ya shilingi milioni 80 kukabiliana na ugonjwa wa kipindu pindu na Chikunguya katika Kaunti ya Mandera.
Aidha, serikali imewaita maafisa wote wa matibabu waliopelekwa kusaidia kupambana na kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola katika nchi za Sierra Leone na Liberia, kusaidia kukabiliana na kuzuka kwa ugonjwa wa Chikunguya humu nchini.