Wakaazi wa eneo la Pwani wametakiwa kuwachagua viongozi watakaowajibikia vyema majukumu yao na kuangazia maslahi ya wananchi ili kuboresha ugatuzi humu nchini.
Akizungumza katika mkutano wa wanawake katika eneo la Majengo mjini Mombasa siku ya Jumanne, Afisa wa Mipango katika Shirika la Muhuri Bi Monica Wanjiru, alisema kwamba ili ugatuzi uwe na manufaa zaidi mashinani, ni lazima wananchi kuwachagua viongozi wenye ari ya kuleta maendeleo kwa jamii.
Bi Wanjiru amewataka wananchi kufanya uamuzi wa busara kwenye uchaguzi mkuu ujao na kuwachagua viongozi watakaoleta mabadiliko katika nchi na wala sio wenye malengo binafsi ya kujinufaisha wao wenyewe.
"Tafadhali wakaazi wa Mombasa kuweni makini wakati wa kufanya maamuzi ya uchaguzi wa viongozi. Wapigieni kura viongozi watakao wasaidia katika maswala ya maendeleo,” alisema Wanjiru.
Mwanaharakati huyo aliahidi kuzuru mashinani na kuielimisha jamii kuhusu jinsi ya kufanya maamuzi bora yatakayoleta manufaa kwa mfumo mpya wa ugatuzi sambamba na maendeleo mashinani.