Wakaazi katika eneo la Spaki, Kaunti ya Mombasa, wameitaka serikali ya kaunti kushughulikia swala la ukosefu wa maji safi katika eneo hilo.
Wakaazi hao walisema kuwa wamekuwa wakitumia maji ya chumvi na kulazimika kununua maji safi kwa shilingi 20 kwa kila mtungi.
Wakiongea na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika eneo hilo, wakaazi hao wakiongozwa na Khalid Yusuf, walisema kuwa shida hiyo inaathiri kazi zao za kujitaftia riziki.
“Bei tunayouziwa maji iko juu sana kwani sio sisi sote tulio na uwezo wa kununua maji hayo kwa bei hiyo kila siku,” alisema Yusuf.
Aidha, wameitaka shirika la maji katika kauti hiyo kufuatilia swala hilo na kupata suluhisho kamili kwa wakaazi hao.
Wakaazi hao walisema kuwa wametembelea ofisi hizo mara kadhaa huku kila mara jibu wanalolipata kutoka kwa maafisa hao likiwa ‘kuweni na subira swala hilo linashughulikiwa’.